Friday, June 22, 2012

KENNETH ASAMOAH ATEMWA YANGA- KLABU KUMLIPA FIDIA

Hatimaye mshambuliaji wa Yanga kutoka Ghana Kenneth Asamoah ametemwa na klabu hiyo baada ya kuitumikia kwa takribani msimu mmoja tu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Yanga, Asamoah amefikia makubaliano na Yanga kwa kulipwa fidia ya kuvunjiwa mkataba wake aliousaini msimu uliopita.

Kenneth Asamoah anaondoka Yanga huku akiwaachia wapenzi wa klabu hiyo kumbukumbu ya goli zuri la kichwa alilowafunga Simba kwenye fainali ya kombe la Kagame mwaka jana kwenye uwanja wa Taifa.

TIMU 20 KUCHEZA LIGI DARAJA LA KWANZA

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeridhia mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ya kutaka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwa na timu 20 badala ya 18 za sasa.

Lengo la mabadiliko hayo ni Ligi ya Taifa (NL) kuchezwa kwa kanda, hivyo msimu huu timu mbili zaidi (ukiondoa tatu ambazo zimeshapanda kutoka NL) zitaongezwa ili kufikisha idadi ya timu 20 katika FDL.

Timu ambazo zimepanda kutoka NL iliyochezwa katika vituo vitatu ni; Kanembwa JKT ya Kigoma iliyoongoza Kituo cha Kigoma, Ndanda SC ya Mtwara iliyoibuka kinara Kituo cha Mtwara na Polisi Mara iliyokamata usukani katika Kituo cha Musoma.

Kamati ya Utendaji pia imepitisha mapendekezo ya kuchezwa play off ili kupata timu mbili zaidi za kucheza FDL msimu huu. Timu zitakazocheza play off katika utaratibu utakaotangazwa baadaye na Kamati ya Mashindano ni tatu zilizoshuka kutoka FDL na tatu nyingine zilizoshika nafasi za pili katika NL kutoka vituo vya Kigoma, Mtwara na Musoma.

Timu tatu zilizoshuka FDL ni AFC ya Arusha, Samaria ya Singida na Temeke United ya Dar es Salaam wakati zilizoshika nafasi za pili katika NL na vituo vyao kwenye mabano ni Kurugenzi ya Iringa (Mtwara), Mwadui ya Shinyanga (Kigoma) na Tessema ya Dar es Salaam (Musoma).

Hata hivyo, timu zitakazoshuka kutoka Ligi Kuu bado zitaendelea kuwa tatu kama ilivyo kwa zitakazopandwa

AWAMA YA KWANZA USAJILI MWISHO AUGOST 10

Kipindi cha kwanza cha usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu wa 2012/2013 kitamalizika Agosti 10 mwaka huu kulingana na kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ya 2012/2013.
Uhamisho wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuacha wachezaji (sio wa Ligi Kuu. Wachezaji wa Ligi Kuu wanacheza kwa mikataba) ni kuanzia Juni 15- 30 mwaka huu.

Kwa klabu za Ligi Kuu kutangaza wachezaji watakaositishiwa mikataba yao ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu na usajili wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu.

Tunasisitiza kipindi cha usajili kiheshimiwe na mikoa yote kwa sababu usajili huo huo ndiyo utakaotumika katika michuano ya Kombe la FA. Kwa maana nyingine hakutakuwa na kipindi kingine cha usajili wa wachezaji kwa klabu zote nchini hadi hapo litakapofunguliwa dirisha dogo.

Mechi ya kufungua msimu ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kati ya mabingwa wa Ligi Kuu, timu ya Simba na makamu bingwa Azam itachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati Ligi Kuu itaanza Septemba Mosi mwaka huu, na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) yenyewe itaanza Septemba 15 mwaka huu.

Ratiba ya Ligi Kuu itatolewa Julai 23 mwaka huu.

MISRI YAOMBA KUIKABILI NGORONGORO HEROES

Chama cha Mpira wa Miguu Misri (EFA) kimeomba mechi mbili za kirafiki kwa timu yao ya vijana na timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (Ngorongoro Heroes).

EFA imeomba mechi hizo zichezwe Julai 3 na Julai 5 mwaka huu kwa masharti maalumu. Ikiwa zitachezwa Misri, mwenyeji (EFA) atagharamia Ngorongoro Heroes kwa malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya kufanyia mazoezi.

Ikiwa mechi hizo zitachezwa Dar es Salaam, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaigharamia timu ya Misri kwa malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya mazoezi. Hivyo kila timu itajigharamia kwa usafiri wa ndege na posho kwa timu yake.

Sekretarieti ya TFF inafanya uchambuzi wa gharama ili kujua ipi ni nafuu kabla ya kufanya uamuzi wa wapi mechi hizo zichezwe.

Ngorongoro Heroes imeingia raundi ya pili ya michuano ya Afrika ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Algeria baada ya kuitoa Sudan katika raundi ya kwanza.

Itacheza mechi ya kwanza ya raundi ya pili Julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itakuwa Agosti 11 mwaka huu nchini Nigeria

Friday, May 25, 2012

SHIJI KAGAWA: KUTOKA LIGI YA PILI YA JAPAN MPAKA DORTMOND-SHIJI KAGAWA SUPERSTAR ANAYEFUATIA NDANI YA MAN UNITED.

 

Wakati taarifa za usajili wake kwenda Manchester United zikizidi kukaribia kuwa ukweli, ebu leo tuangalie uchambuzi wa kisoka kuhusu Shinji Kagawa.

Misimu miwil iliyopita, Shinji Kagawa alikuwa hajulikani kabisa nje ya Japan, lakini watu wale wenye macho yanayoona mbali waliona kiungo aliyebarikiwa uwezo wa kucheza soka huku akiisadia klabu yake ya Cerezo Osaka kupanda daraja la juu kwenye soka la Japan ndani ya misimu mitatu tu. Sasa yupo karibuni kujiunga na mabingwa kihistoria wa Barclays Premier league pale Theatre of Dreams - baada ya Red Devils kutuma ofa ya £13miilion kwa Dortmund.

Kagawa alikuwa ndio mjapan wa kwanza kuisaini mkataba wa level ya proffessional kabla ya kumaliza kutoka kwenye elimu ya juu ya sekondari. Akiwa na miaka 18 aliweza kupata nafasi ya kwenye kikosi cha kwanza cha Cerezo, na kujiamini kwake kukapanda sana baada ya kuwa na rekodi nzuri ya kufunga. Kagawa alifunga mabao 27 katika mechi 44 kwenye msimu wa 2009 na kuwasaidia Cerezo kurudi kwenye ligi kuu ya Japan baada ya kushuka kwa miaka 3. Lakini hakuweza kucheza sana kwenye ligi kuu ya Japan, baada ya wakala wa kijerumani Thomas Kroth kushughulikia uhamisho  ambao ulimuamisha kinda hilo kwenda Borussia Dortmnund - wakati timu hilipokuwa ikijipanga upya baada ya kumaliza ligi kwenye nafasi ya 5.

Performance yake pale Dortmund inajieleza yenyewe; kwenye msimu wa kwanza barani ulaya, Kagawa alikuwemo kikosi bora ya Bundesiliga japokuwa alitumia nusu ya msimu kuwa nje ya dimba kutokana  na majeruhi. Mwaka huu, ameweka rekodi mpya kwa Wajapan waliowahi kucheza Ulaya kwa kufunga mabao 13 kwenye mechi 32. Shinji ni hatari kila anapogusa mpira, ana uwezo wa kutengeneza nafasi kwa kutoa pasi za mwisho huku akiwa na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti ya mbali.


Nchini kwao Japan, Kagawa ni moja ya wanasoka wenye majina makubwa sana na mara nyingi amekuwa akitumika kwenye matangazo akitangaza vinywaji pamoja video games.

Jezi yake ndio inaongozwa kwa kuuzwa, kwenye msururu wa maduka ya kuuza vifaa vya soka KAMO, huku ikitegemewa mauzo kupanda ikiwa tu atajiunga na klabu yenye umaarufu mkubwa kuliko zote duniani huko ASIA - Manchester United. Umaarufu wa Kagawa ambao kwa sasa upo sawa na wachezaji kama Yuto Nagamoto wa Inter pamoja na mshambuliaji wa CSKA Moscow Keisuke Honda.

Lakini tofauti na wenzake Nagamoto na Honda ambao wanapenda sana kutokea kwenye vyombo vya habari, Kagawa yeye ni kama Paul Scholes hapendi mambo ya kuwa karibu sana na media kwa aibu aliyonayo.

Pamoja na kuwa na miaka miwili Ujerumani, bado anaongea aidha kupitia mtafsiri wake au vyombo vya habari vya Japan ambavyo vimekuwa vikimfuata.

Ikiwa atahamia England itabidi ajipange sana ama aendelee kuufuata mfano wa Paul Scholes ili aweze kuepukana na vyombo vya habari vya nchi hiyo ambavyo vingine vimeanza kusema United wanamsajili Mjapan huyo kwa sababu za kibiashara - kuongeza mauzo ya bidhaa zao barani Asia hasa nchini Japan. Lakini  ama kwa hakika huyu ni aina ya kiungo mshambuliaji ambaye United wanamhitaji ili kuweza kukirudishia kikosi uwezo wa kutawala tena soka la England.

Ndani ya misimu miwili aliyokaa na Dortmund - amesaidia klabu hiyo kuupora utawala wa soka la Ujerumani kutoka kwa Bayern Munich kwa mara mbili mfululizo.

SIENDI POPOTE-GYAN

 

Gyan
Asamoah Gyan
Mshambuliaji wa Sunderland Asamoah Gyan ametupilia mbali taarifa zinazosema anahama, akisema hana mpango wa kuondoka.
"Siondoki Sunderland, sibabaishwi na uvumi uliozagaa katika magazeti na tovuti," amesema Gyan akizungumza na tovuti ya MTNFootball.com.
Gyan kutoka Ghana, alifunga magoli 11 katika msimu wake wa kwanza katika ligi ya England.
"Nimejitolea kuichezea Sunderland kwa sababu napenda klabu na utamaduni wake," amesema Gyan.
"Nitabakia Sunderland msimu ujao, na katika siku zijazo, na nasubiri kwa hamu kukutana na wachezaji wenzangu na mashabiki wa Sunderland, tutakaporejea mwezi ujao."
Gyan ni mchezaji wa bei ghali zaidi kununuliwa na Sunderland, akitokea klabu ya Rennes ya Ufaransa kwa kitita cha zaidi ya pauni milioni 13, mwezi Agosti mwaka 2010.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Sunderland, kutokana na mtindo wake na ufungaji wa magoli muhimu, likiwemo goli la kusawazisha katika dakika za majeruhi dhidi ya Newcastle mwezi Januari 2011.