KOCHA wa Simba, Milovan Cirkovic, amepanga kufanya marekebisho kwenye safu ya ulinzi kwa kusajili mabeki imara zaidi.
Milovan ambaye timu yake iliichapa Yanga mabao 5-0 juzi Jumapili sambamba na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, alisema kuwa nafasi nyingine hana matatizo nazo ingawa anafikiria pia kuzigusa.
"Kwa sasa nitafanya mabadiliko kidogo kwenye safu ya ulinzi kwa kuongeza nguvu zaidi. Hiyo ndiyo sehemu ambayo imekuwa na matatizo kwenye mechi zetu," alisema.
"Nitaimarisha zaidi beki, nahitaji timu imara zaidi, hizo idara nyingine nitafanya tathmini ya kina na ninaweza kuzigusa kidogo, lakini hazina matatizo sana kama kwenye ulinzi."
Kwa sasa Milovan anaiandaa timu yake kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy itakayofanyika Ijumaa huko Sudan.
Katika mechi ya awali Simba ilishinda mabao 3-0 jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa duru za ndani za Simba, Milovan atamtema beki wa Uganda, Derrick Walulya na pengo lake kuzibwa na beki mwingine wa kigeni.
Tayari Simba imemsajili kiungo wa Uganda, Mussa Mudde.
No comments:
Post a Comment